Mkuu
mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk
Fredrick Shoo jana, mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alielezea
kushangazwa kwake na kile alichokiita “jeshi kuingizwa ndani ya Ukumbi
wa Bunge la Jamhuri mjini Dodoma”.
Alisema hayo mjini hapa alipokuwa akitoa hotuba yake ya kwanza mara
baada ya kuingizwa kazini kushika wadhifa huo atakaoutumikia kwa miaka
minne.
Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, anachukua nafasi ya
Askofu Dk Alex Malasusa ambaye amemaliza muda wake wa uongozi.
Hafla hiyo ambayo Majaliwa alikuwa mgeni rasmi, ilihudhuriwa pia na
mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na maaskofu
zaidi ya 28.
Akizungumza kwa hisia, Askofu Dk Shoo alionekana kuguswa na mambo matano yaliyojitokeza katika Taifa.
Polisi bungeni
Alieleza kutoridhishwa kwake na mwenendo wa Bunge, akisisitiza kuwa ni lazima mihimili mitatu ya dola ijiendeshe kwa uhuru.
“Iachiwe ifanye kazi yake kwa uhuru na kila mhimili utunze heshima hiyo.
Tunasikitishwa sana na hali inayoendelea katika Bunge letu na nashukuru
nimewaona baadhi ya wabunge humu,” alisema.
Wabunge waliokuwapo ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe, Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael, Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema Anthony Komu wa Moshi Vijijini, James Mbatia wa
Vunjo na Lazaro Nyalandu wa Singida Kaskazini.
“Hili ni lenu na Spika wenu (akiwageukia wabunge). Bunge ndiyo nyumba ya
demokrasia kama kweli Tanzania tunataka kujenga jamii ya kweli ya
inayoheshimu misingi ya kidemokrasia. Sisi tunatarajia kuona na kusikia
hoja zikijadiliwa kwa uwazi na katika hali ya kistaarabu. Kwa
kuchezeachezea heshima hii ya Bunge sasa tunaona juzijuzi tu jeshi
linaingia bungeni. Nyumba ya demokrasia haiingizwi majeshi. Kwa hiyo
wabunge tunzeni heshima yenu,” alisema na waumini wa kanisa hilo
kumshangilia.
Utumbuaji majipu
Askofu huyo wa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alimpongeza Rais John
Magufuli, Waziri Mkuu, Majaliwa na timu yao kwa namna walivyoanza vizuri
katika utawala wa awamu ya tano.
“Rais ameshaweka wazi kwa wananchi nia yake ya kufufua uchumi na
kupambana na ufisadi. Katika muda mfupi huu wa uongozi wake,
mmekwishakuanza (Waziri Mkuu) kutumbua majipu makubwa ya ufisadi,”
alisema na kuongeza:
“Tunamwomba sana Rais na timu yake aendelee kutumbua majipu hayo kwa
ujasiri mkubwa na miji ya majipu hayo ioshwe na kukamuliwa ili
yasirudie.”
Hata hivyo, alitahadharisha kuwa utumbuaji huo unatakiwa ufanyike kwa
hekima na misingi ya uwazi, ili wasio na nia njema wasitumie kuwakomoa
wasio na hatia.
“Yale majipu ambayo ni hasa, hayo yasiachwe kutumbuliwa na msiwe na hofu
yoyote kutoka kwa watu watakaowapinga, najua kuna watu wanajipanga
kuwapinga, msiwe na hofu yoyote,” alisema Askofu Shoo.
Mkwamo Zanzibar
Akizungumzia mkwamo wa kisiasa visiwani baada ya Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi na kutangaza tarehe ya kuurudia, Askofu
Shoo alisema yanayoendelea huko yanalitia doa Taifa.
“Tunamuomba pia Mungu awape hekima na ujasiri wa kushughulikia suala la
Zanzibar ili maridhiano na haki itendeke na nchi yetu iendelee kuwa na
utulivu na amani. Mambo yanayoendelea kule Zanzibar yasipodhibitiwa
vizuri yataweza kutia doa Awamu ya Tano ya uongozi.”
Katiba mpya
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Askofu Shoo alisema hayo ndiyo matarajio
makubwa ya Watanzania ambao wanataka kuona Serikali ya Awamu ya Tano
ikiwatimizia ndoto hiyo.
“Tunazidi kumuomba Mungu. Matarajio ya Watanzania ni uwapo wa Katiba
Mpya inayoheshimu matakwa ya wengi na inayosisitiza utawala wa sheria na
haki za kibinadamu,” alisema na kuongeza:
“Ninashauri mchakato wa Katiba Mpya ufikiriwe kwa upya na utumike kama
njia ya kuganga madhaifu na majeraha yaliyotokea au ambayo yapo katika
awamu zote zilizotangulia.”
Ada elekezi
Akizungumzia ada elekezi kwa shule za binafsi, Askofu Shoo alitaka suala
hilo litizamwe upya tena kwa kuwashirikisha wadau wa elimu nchini.
“Nina imani Serikali ikiboresha shule zake hakutakuwa na haja ya kuweka
ada elekezi. Tunachohitaji katika ubora wa elimu ni kuanzisha mamlaka
inayojitegemea ya ithibati na udhibiti. Kuwa na mamlaka hiyo na
ikijitegemea naamini kutaleta mafanikio katika ubora wa elimu.”
Waziri Mkuu
Akihutubia kwa niaba ya Rais, Majaliwa alisema wabunge wanapaswa kuwa kioo cha jamii.
“Ulipozungumzia hili ulizungumzia Bunge na mimi nashukuru umelieleza
hilo la wabunge wenzangu. Jambo hilo ni letu, tutahakikisha suala la
demokrasia linaimarishwa ndani ya Bunge,” alisema.
“Lakini pia nataka nieleze Bunge ni eneo ambalo linaweza kuijenga jamii
hii mpya. Wabunge ni kioo, ni watu wa kuigwa. Hivyo ni vyema tukalitumia
Bunge kwa lugha sahihi na tabia nzuri. Tutaendelea kusimamia lugha
nzuri ndani ya Bunge ili wanaoona waweze kuiga. Niwahakikishie
Watanzania tutaendelea kuzungumza na wabunge ili bungeni pawe mahali
panapojenga tabia njema,” alisema.
Kuhusu Katiba Mpya, alisema hoja ya Askofu Shoo ifanyiwe kazi na
akadokeza kuwa amekuwa akizungumza na wabunge juu ya suala hilo.
“Suala la ada elekezi kwa shule binafsi litazungumzwa na wadau wote ili
kutoa mwelekeo sahihi. Nataka nikuahidi Baba Askofu, tutaziboresha shule
zote za umma ili ziweze kutoa elimu bora,” alisema.
Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Issac Aman alisema kama kuna jipu
linalopaswa kutumbuliwa, basi ni la Watanzania kukosa moyo wa uzalendo.
Askofu huyo alisema ufisadi na ubinafsi unaofanywa na baadhi ya Watanzania ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo na uadilifu.
|