.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

Monday, November 10, 2014

Makinda kumzika Sata

Makinda kuongoza ujumbe wa Bunge la SADC kumzika Rais Sata kesho Mjini Lusaka , Zambia  

Na Owen Mwandumbya, Lusaka Zambia

Rais wa Bunge la SADC ambaye pia ndiye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda kesho tarehe 10 Novemba, 2014 ataongoza ujumbe wa Bunge la SADC kushiriki Misa Maalum ya kuombea mwili wa aliyekuwa Rais wa Zambia marehemu Michael Chilufya Sata katika misa maalum itakayofanyika katika viwanja vya Makumbusho Mjini Lusaka, Zambia.

Katika ujumbe huo wa Bunge la SADC, Makinda ataongozana na viongozi wengine wa Bunge hilo ambao ni Spika wa Zimbabwe Mhe. Jaji Jacob Mudenda, Spika wa Bunge la Afrika Kusini Mhe. Baleka Mbete, Spika wa Bunge la Malawi Mhe. Richard Msowoya Spika wa Bunge la Angola Mhe. Fernando da Piedade Dias dos Santos na Mwenyeji wao Spika wa Zambia Dkt. Patrick Matibini.

Kutoka secretariat ya makao makuu wa Bunge hilo, katibu Mkuu wa Bunge Bunge la SADC Dkt. Essau Chiviya ataambatana na ujumbe huo kuwakilisha sekretariati ya Bunge hilo katika Misa hiyo Maalum Mjini Lusaka, Zambia.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali iliyotolewa na Serikali ya Zambia, Misa hiyo Maalum ya kuombea mwili wa Rais Rata itanyika kesho tarehe 10 Novemba, 2014 na inatarajiwa kuhudhuriwa na Marais kutoka kila kona ya dunia pamoja na viongozi mbalimbali wa Kimataifa watakaoziwakilisha nchi zao kabla ya kufanyika kwa mazishi yake ambayo yamepangwa kufanyika siku ya jumanne tarehe 11 Novemba, 2014 jijini Lusaka.

Sata aliyekuwa na umri wa miaka 77 alifariki tarehe 29 Oktoba, 2014  jijini London Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu ambapo kifo chake kilitokea siku chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo, sherehe ambazo hakuweza kushiriki kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

 Mwanasiasa huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya kuongoza chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party Democracy, kikiwa madarakani kwa miaka ishirini.

Sata ambaye alibatizwa jina la "King Cobra" na wafuasi wake wakati alipochaguliwa mwaka 2011, alionekana kama mbadala wa siasa za Zambia na mtu ambaye alikuwa wavitendo licha ya kukosolewa kwa sehemu kubwa na upinzani.

Makinda na ujumbe wake wanatarajia kurudi nchini siku ya jumatano baada kushiriki pia mazishi yatakayofanyika tarehe 11 Novemba, 2014.