.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

Tuesday, April 1, 2014

Tuchangamkie mpango wa TIKA-Magalula

 Ofisa Masoko na Elimu kwa Umma kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bi. Grace Michael akimshukuru mgeni rasmi kwa hotuba nzuri kuhusu mwito wa kujiunga na Bima ya Afya na kutibiwa kwa Kadi almaarufu Tiba kwa Kadi (TIKA)



MKUU wa Mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula amezindua rasmi mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii ujulikanao kama Tiba kwa Kadi (TIKA) huku akiwataka wadau kuhakikisha wanapitisha mpango huo kwa maslahi ya wananchi wa mkoa huo.
Magalula ameyasema hayo wakati akizindua mpango huo kwa wadau mbalimbali kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo amesisitiza kuwa bila ya wananchi kujiunga katika  utaratibu wa TIKA itakuwa ni vigumu kumudu gharama za matibabu ambazo zinaongezeka kila kukicha.
“Jamani wenzetu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wametuletea mpango huu ni vyema tukaujadili kwa makini na kwa mtazamo chanya ili hatimaye Halmashauri ya Mji ianze utekelezaji wa suala hili…utaratibu wa kuchangia kabla ya kuugua ni mzuri na unakupa uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiingia kwenye matatizo mbalimbali yakiwemo ya madeni ama kuuza vitu vya nyumbani kwa ajili ya kupata fedha za matibabu hali ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa familia husika hivyo akasisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa TIKA ili kuondokana na matatizo hayo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa hakusita kuutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha unabadilika au kubadili mbinu zake za uhamasishaji kwa kuwafuata wananchi ambao wako katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji mbinu ambayo itarahisisha kuwafikia wananchi wengi zaidi na uchangiaji wake utakuwa ni rahisi tofauti na kumfuata mtu mmoja mmoja. 
“Endeleeni na uboreshaji wa huduma za matibabu na kuangalia ni namna gani mtamaliza au kupunguza tatizo la ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ili wananchi wasiwe na visingizio wakati wa kujiunga na mipango kama hii,” alisema.
Aidha aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kuweka utaratibu mzuri wa uwekaji wa kumbukumbu za wanachama kwa kuwa ndizo zinazotoa picha halisi ya mahitaji yaliyopo ndani ya halmashauri ama mkoa kwa ujumla.
Akizungumzia uboreshaji wa huduma za afya ndani ya Halmashauri hiyo, alimwagiza Mganga Mkuu kutumia fursa zinazotolewa na NHIF za mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo kwa lengo la uboreshaji wa huduma za matibabu.
“Mbali na fursa ya mikopo hii pia ni vyema matumizi ya fedha zitokanazo na CHF/TIKA  i zikatumika kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo asilimia 67 itumike kwa kununulia dawa, asilimia 15 itumike kwa uboreshaji wa huduma za afya na inayobaki ndo inaweza kutumika kwa shughuli zingine ambazo zinahusiana na masuala ya afya,” alisema.
Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao uliwakilishwa na Meneja wa CHF, Constantine Makalla alisema kuwa lengo la Mfuko ni kuhakikisha kila halmashauri inaanzisha na kutoa huduma kwa kuwa na sheria ndogo ambapo hadi Desema 31, 2013 jumla ya Halmashauri 128 zilikuwa na sheria ndogo.
Alisema kuwa mipango ya NHIF kwa mwaka huu ni kuongeza uwigo wa wanachama, kuanza utaratibu wa kuzizawadia Halmashauri zinazofanya vizuri na uboreshaji wa daftari la CHF/TIKA na taarifa za wanachama wake nchi nzima.


 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula akifungua mkutano wa wadau mkoani Geita unatakaojadili mchakato wa uanzishaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii ujulikanao kama Tiba kwa Kadi (TIKA).


 Katibu Tawala wa Mkoa  Severine Kahitwa akieleza umuhimu wa kuwa na utaratibu wa TIKA ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita.


 Wadau wa mkutano huo wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mkuu wa Mkoa huo.

  Sehemu ya wadau wakisikiliza maagizo kutoka kwa mgeni rasmi ya namna ya kujadiliana katika mkutano huo. 

 Mkutano huo pia haukuwanyima fursa ya kuelewa kinachozungumzwa ndani ya kikao hicho walemavu wa kusikia, mbele ni mkalimani wa walemavu hao John Mukube.

Mkuu wa Mkoa Magalula Said Magalula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya kundi maalum ambalo nalo limeshiriki mkutano huo.

Wadau wakiwa makini kusikiliza mada zilizowasilishwa kwa ajili ya uanzishwaji wa TIKA mjini Geita



 Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja.


Wajumbe wakipitia mada zilizoandaliwa katika mkutano huo.