Na Frank Mvungi-Maelezo
Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA)
imedhamiria kufungua Ofisi za Kutolea huduma za hali ya Hewa ili kupunguza
ajali katika maziwa hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam
na Meneja wa Huduma za Utabiri wa TMA Bw.
Samwel Mbuya wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeona
kuna umuhimu wa kujenga vituo vya kutoa huduma za Hali ya hewa nchini katika
maziwa ya Victoria,Tanganyika na Nyasa, vituo hivi vitasaidia kwa kiasi kikubwa
kupunguza ajali kwa kuwa tutafunga vifaa vya kisasa vya kupima hali ya hewa
Alisema Mbuya.
Aidha Mbuya amesema kuwa TMA imeendelea
kuboresha huduma za utabiri wa Baharini kwa kuweka maboya maalum katika ukanda
wa bahari ya Hindi pamoja na kufungua kituo cha hali ya hewa katika Bandari ya
Zanzibar.
Mbuya alibainisha kuwa kwa upande wa
usafiri wa anga TMA imeendelea kutoa huduma zenye kukidhi vigezo vyenye hadhi
ya Kimataifa ili kuleta usalama kwa watumiaji wa Usafiri huo nchini.
Akizungumzia kuhusu uboreshaji wa
mtandao wa vituo,Mbuya alisema kuwa hivi sasa mtandao huo umeongezeka ikiwemo
kusimikwa kwa rada mbili za hali ya hewa moja ipo katika eneo la Bangula-Dar es
salaam na nyingine iko katika hatua za mwisho huko Kiseke-Mwanza.
Pia Mbuya aliongeza kuwa Mamlaka hiyo
imefanikiwa kuongeza wigo wa usambazaji taarifa zake hadi kufikia zaidi ya
radio 40 za kijamii lengo likiwa ni kuwafikia wananchi waliopo vijijini.
Dira ya TMA Inalenga kuhakikisha kuwa
ifikapo mwaka 2015 Mamlaka hiyo inatoa huduma katika viwango vya Kimataifa.