Kamati
ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum Kuhusu Kanuni za Bunge Maalum
imemaliza kazi yake na kuwasilisha Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum 2014.
Akiwasilisha
Taarifa ya Kamati hiyo kwenye semina ya Wajumbe wa Bunge Maalum, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Profesa Costa
Ricky Mahalu amesema kazi ya Kamati yake ilifanyika kwa muda wa siku sita kwa
kupitia na kuchambua kwa kina rasimu ya Kanuni za Bunge iliyokuwa imeandaliwa
na Kamati ya Maandalizi ya Bunge Maalum chini ya usimamizi Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar.
Kamati
hiyo imepitia Sehemu zote kumi na moja za rasimu ya awali na kushauri marekebisho
na mapendekezo mbalimbali ambayo yatapitiwa na wajumbe wote wa Bunge Maalum
kabla ya kupitisha Azimio la kuridhia
Kanuni za Bunge Maalum. Kupitishwa kwa
Azimio la Kanuni hizi kutawezesha uchaguzi wa Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge
Maalum pamoja na utaratibu wa Kiapo kwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum,
kiapo kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum , kiapo kwa Wajumbe
wa Bunge Maalum na hatimaye uwasilishwaji na mjadala wa rasimu ya Katiba.
Aidha, Kamati imependekeza kuwa kura zote zitakazopigwa ziwe za siri.
Aidha,
Kamati imepekeza kuwa Siwa itakayotumika katika Bunge Maalum ihifadhiwe baada
ya kupatikana kwa Katiba mpya ili iwe ukumbusho wa kihistoria. Siwa hiyo iwe na kichwa cha dhahabu, kitabu
(kuashiria Katiba), alama ya watu wa makundi mbalimbali, rangi za taifa, nembo
ya taifa na alama ya kalamu kama kielelezo cha uandishi.
Baada
ya taarifa kuwasilishwa Semina iliahirishwa ili kutoa fursa kwa wajumbe
kuipitia rasimu mpya ya Kanuni na kujiandaa kwa mjadala.
Taarifa
na matukio zaidi tembelea Kituo cha Habari , Maktaba ya Picha katika tovuti
hii.
|