KATIKA moja ya hotuba za hayati Baba wa Taifa Mwlimu Julius Kambarage Nyerere
aliwahi kusema kuna baadhi ya mambo hapa nchini ukitaka kuyahoji lazima uwe na
moyo mgumu kama wa mwendawazimu hivi.
Kwa sasa moja ya mambo hayo ni elimu: elimu ya awali; elimu ya msingi;
elimu ya sekondari; elimu ya vyuo. Zamani ili shule ihesabike na hata
kusajiliwa kama shule kuna mambo mengi yalihitajika likiwemo la uwanja wa
michezo na shamba la shule. Siku hizi ni dhambi ya mauti kuzungumzia shamba la
shule tena mzazi akikuskia achilia mbali mwalimu! Mwanafunzi ndiyo kabisa
atatamani umwagiwe tindikali!
Siku hizi mtoto anafanyiwa kila kitu
awapo shuleni. Kuna watu wa kufanya usafi ndani na nje ya vyumba vya madarasa,
, kupika, basi la kumbeba na kurudisha nyumbani, akifika nyumbani kuna
msaidizi/mfanyakazi wa nyumbani wa kumfulia hadi nguo za ndani, kumpikia,
kumtandikia kitanda na kunyooshea nguo. Shuleni shamba darasa tena hakuna. Zamani
katika orodha ya vifaa vya kwenda navyo shuleni jembe kilikuwa kifaa
kimojawapo. Siku hizi dhubutu! Kiwanja cha michezo si sharti muhimu tena. Hali
hii iko tangu shule ya awali hadi chuo kikuu! Ni dhahiri maandiko haya
hayatabadilisha chochote kwa wakati huu lakini yataonekana ya maana Wachina
watakapoanza kuchangamkia hata kazi za majumbani hapa Tanzania kwani wao
wamefundishwa maana ya kazi kwa vitendo.
Serikali, wazazi, wadau wako wapi kudai
na kuhimiza kazi za mikono katika shule zetu? Shule yoyote kabla ya kusajiliwa
ioneshe japo shamba darasa mahali wanafunzi watajifunza kwa vitendo kupanda na
kuvuna mchicha. Wanafunzi wafundishwe kufanya usafi kwa vitendo kwa mfano
kufagia darasa, kuokota takataka, kukata kucha, kuosha sahani yake anapomaliza
kula, kutoa buibui na nyinginezo. Wakiwa majumbani wajifulie ngou zao wenyewe,
wafanye usafi, wajifunze kupika, wanyooshe nguo zao wenyewe, watengeneze
bustani na kuzimwagilia inapobidi, wahimizwe maswala ya kiroho, kwa kifupi
wafundishwe kuwajibika.
Jeshi la Kujenga Taifa ndilo lilikuwa
limesalia ili kuziba ombwe hili. JKT halipo tena. Na hata ikitokea likawepo halitokuwa
tena kama la opereshini miaka 30
(waliopita jeshini wanaelewa operesheni).
Ole wetu! Ole wa Taifa hili!.Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani
Tanzania, Dkt. Joyce Ndalichako alinukuliwa akilalamika kwamba wanafunzi
waliandika mashairi ya Bongo flavor kwenye
mitihani! Kumbe waandike nini? Nyimbo za makuzi shuleni siku hizi hakuna tena.
Nyimbo za kizalendo na ukakamavu ni historia mashuleni! Kibaya zaidi hata Wimbo
wa Taifa umebaki kuchezwa mkanda tu uliorekodiwa
halafu wanafunzi wanasikiliza!
Mustakabali wa Taifa uko wapi! Tusipojenga msingi imara tusishangae nyumba
kuporomoka kwani Walatini wanasema volenti
non fit injuria! (lakijitakia halina madhara). Tumeyataka wenyewe!
Tuna wakaguzi waliosoma. Hivi hawa wanakagua nini? Mwandiko
mzuri? Mwalimu kumaliza silabasi? Wadau nisaidieni. Mada ni pana. Mtoto huyu
akimaliza shule (darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita, shahada ya
kwanza) anakuwa ni mzigo usiobebeka pande zote. Si kwa wazazi, si kwa serikali!
Hawezi kufanya kitu chochote! Hajafundishwa kufanya hivyo! Hajalelelwa katika
mazingira hayo! Hana pa kuanzia. Dhana ya kilimo kwanza kwake ni msamiati usio
na mashiko. Likitokea la kutokea kwamba mzazi amefariki dunia huu unakuwa ni
mwanzo wa mwisho wa mtoto huyu! Ataanza kujioanisha na mazingira yatakayomfaa (to search for identity). Atayapata
mazingira hayo au kwa watumia dawa za
kulevya kwa wavulana au kwa kupiga umalaya kwa wasichana. Hapa tusiulizane
madhara yake nini.
Laiti mtoto huyu angelikuwa anajua kujitegemea japo kidogo tu
angeyamudu maisha. Angekuwa mnyenyekevu. Kwa bahati mbaya kila mtoto anaota
kwenda Ulaya tena kwa gharama yoyote ile. Mzazi atafanya kila linalowezekana na
lisilowezekana, mtoto atahonga hata visivyohongeka ili mradi aende Ulaya!
Kufanya nini? Sina jibu.
Sera ya elimu iangaliwe upya. Shule zote (binafsi na serikali)
ziwekewe vigezo. Tusiogope kujifunza kutoka mahali pengine. Kwa mfano shule za
seminari zinaongoza kwa kufanya vizuri. Lakini hapa ni mahali wanafunzi wanafanya
kazi zote peke yao. Wana mashamba yao wanayolima na kuvuna wenyewe, wanafanya
usafi wa mazingira na vyumba vya madarasa yao, kwa kifupi wanajitegemea
wakiongozwa na nidhamu ya hali ya juu. Haijawahi kutokea mtoto aliyemaliza
masomo katika shule hizi akawa tegemezi kiasi cha kutobebeka. (kwa ujasiri
naruhusu changamoto/challenge kwa hili kutoka wa mtu yeyote). Huu ni ushahidi
kwamba inawezekana.
Tujenge msingi imara ili kuwa na taifa imara.
0713 123
254