|
|
|
TAARIFA
KWA UMMA
UKWELI KUHUSU MWANASHRIA
MKUU WA ZANZIBAR MHE. OTHMAN MASOUD OTHMAN
KUAMBATANA NA ULINZI KATIKA
MAENEO YA
BUNGENI MAALUM.
Kumekuwa na
Taarifa potofu zinazosambazwa na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii ya
kuwa “Mwanasheria Mkuu Zanzibar Othman Masoud Othman amekamatwa baada ya kupiga kura ya hapana Bungeni leo”
Tunapenda
kuutarifu Umma wa Watanzania kuwa, taarifa hizo sio sahihi na ni porojo zenye
kutaka kuleta hisia potofu kwa wananchi kuhusu kiongozi huyo.
Ukweli wa Jambo
hili ni kuwa Mhe. Othman Masoud
Othman ametekeleza haki yake ya Kidemokrasia
ya kupigia kura Rasimu ya Katiba inayopendekeza katika Bunge Maalum
leo. Ambapo katika kura alizopiga,
ameweza kuzikubali baadhi Ibara na kuzikataa ibara nyingine katika rasimu ya
Katiba inayopendekezwa.
Pengine hatua hiyo
ya kuzikataa baadhi ya Ibara, haikuwafurahisha baadhi ya Wajumbe na hivyo
kuleta majibishano ndani ya Bunge Maalum wakilalamikia uamuzi wake huo.
Kutokana na hofu
hiyo ya baadhi ya Wajumbe kuanza kupinga uamuzi wake huo ndani ya Bunge, Ofisi
ya Bunge Maalum kama ilivyokawaida kwa kila mjumbe, imeweza kumpatia Ulinzi
Maalum wakati akitoka Bungeni hadi alipoondoka katika viwanja vya Bunge ili
asiweze kubugudhiwa kwa namna yoyote ile kutokana na uamuzi wake huo.
Suala hili
limechukuliwa kipropaganda na kuanza kueneza uongo katika mitandao ya kijamii
kuwa Mhe. Othman amekamatwa baada ya kupiga kura ya hapana.
Tunapenda
kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Mhe. Othman hajakamatwa bali alipewa ulinzi
katika Maeneo ya Bunge Maalum jambo ambalo hufanyika kwa kila mjumbe ambaye kwa
namna moja ama nyingine itaonekana kuna dalili za kubugudhiwa katika Maeneo ya
Bunge kutokana na uamuzi au kitendo alichofanya. Na kutokana na hali ilivyo,
ulinzi wake umeimarishwa pia mahali alipo kwa hivi sasa mpaka atakapomaliza
kazi yake hapa Dodoma.
Kanuni za Bunge
Maalum zimempa madaraka Katibu wa Bunge Maalum kusimamia masuala yote ya Ulinzi
na Usalama kwa Wajumbe na Maeneo yote ya Bunge Maalum.
Imetolewa na Idara ya Habari
Ofisi ya Bunge Maalum
Dodoma
1 Oktoba, 2014