.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

Tuesday, June 12, 2012

Kada ya kati imesahaulika?


Na Prosper Minja

KATIKA makala yangu ya “Elimu kwa vitendo shuleni iko wapi?” iliyochapishwa kwenye gazeti hili la Raia Mwema la Mei 16 –Mei 22, 2012 toleo namba 239 watu wengi waliichangia mada hiyo. Nawashukuru kwa kutoa mawazo mazuri ya kutaka kuondokana na ujenzi wa taifa la walemavu wa viungo na akili. Makala ya leo bado inajikita tena katika eneo hili la mfumo wa elimu Tanzania.

Katika miaka ya hivi karibuni Tanzania inashuhudia mabadilko makubwa katika mfumo mzima wa elimu unaosukumwa na utandawazi. Tofauti na ilivyozoeleka, vyuo vya elimu vya kada ya kati vilivyokuwa vimeanzishwa kwa makusudi maalum sasa vinapoteza ule umaana wake uliokuwa umekusudiwa.  Sina hakika sana na mfumo mzima wa elimu hapa nchini kwa sasa, ila wadau wenye uelewa naomba tusaidiane katika hili.

Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, vilianzishwa vyuo mbalimbali kwa ajili ya kada ya kati. Vilianzishwa vyuo vya elimu ya Ufundi magari/mshine, Uashi, Usimamizi wa Fedha, Elimu ya Bishara, Ufundi Mchundo, Uhazili, Ustawi wa Jamii, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Sanaa,Useremala, msururu ni ndefu. Chuo KIkuu kilianzishwa kimoja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hiki kwa wakati na mazingira ya wakati wa ule kilikidhi mahitaji ya watanzania na nje ya Tanzania.

Tayari mfumo wa elimu ulikwishawekwa bayana. Mtoto ataanzia shule ya awali (chekechea), atakwenda shule ya msingi kwa maana ya darasa la kwanza hadi darasa la saba (enzi za mkoloni ilikuwa ni la nne) na hapa kwa vyovyote vile si wote wangeweza kuendelea na masomo ya sekondari kwa maana ya kidato cha kwanza (au darasa la tano kwa enzi za mkoloni).  Vyuo vya kada ya kati viliandaliwa mahususi kuwapokea hawa  wasioweza kuendelea na masomo ya sekondari ambao katika hali yoyote ile ni wengi kwa kulinganisha na wale waliokwenda kwenye shule za sekondari.

Halikadhalika si wote waliomaliza kidato cha nne walioweza kuendelea na kidato cha tano. Sanjari  na wazo la awali vyuo vya kada ya kati vilikuwa vimeandaliwa kulipokea kundi hili pia ambalo kwa vigezo vyovyote ni kundi kubwa na lenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kutenda. Na ni katika mantiki hiyo pia tunakubaliana tena kwamba si wote waliomaliza kidato cha sita waliweza kuendelea na masomo ya chuo kikuu. Ifahamike hapa kuwa swala kubwa ni uwezo wa kuyamudu masomo na si vinginevyo. Kundi hili nalo lilipata nafasi katika vyuo vya kada ya kati. Hii iliwezekana kwa kuwa tangu zama hizo hadi sasa  mfumo wa elimu kuanzia chini hadi juu una umbo la pyramid: kwa maana kwamba unavyokwenda juu idadi ya wanafunzi inazidi kupungua. Huu ndiyo ukweli na hakuna jinsi ya kuupinda au kuuchakachua.

Vyuo vya kada ya kati vilitoa vyeti mbali mbali vilivyomtambullisha mhitimu pamoja na kazi anayoweza kuimudu.Leo maandalizi ya kada hii ya kati yanapoteza mwelekeo. Sina hakika kama msisitizo wa kujenga vyuo vya namna hii upo tena. Huenda msukumo huu umeelekzwa kwa sekta binafsi. Lakini tukumbuke kwamba sekta binafsi lengo lake ni kufanya biashara na kupata faida na si vinginevyo. Vyuo hivi vilikuwa vinabeba mzigo mkubwa kuliko vyuo vikuu vyote hapa nchini tukivichanganya pamoja.

Matokeo yake kila chuo cha kada ya kati sasa hivi kinataka kusomesha na kutoa shahada (degree) kwa wanafunzi wake. Kuanzia Hombolo, Mipango, Ustawi wa Jamii, Ufundi, Usimamizi wa Fedha, Elimu ya Biashara, Kilimo, msrururu ni mrefu - vimeruhusiwa kutoa shahada za Chuo Kikuu! Kesho akija mtu ofisini kuomba kazi atakupa cheti cha shahada ya kwanza ya useremala kutoka Chuo (Kikuu?) cha Mbuyuni! Wote hawa sasa wana shahada za vyuo vikuu!

Tulichekelea watoto wa chekechea walipoanza kuvaa majoho “wanapohitimu”! Leo hii kila anayehitimu chochote anataka na tunamshangilia akilivaa joho! Nasema nisaidieni pengine huu ndiyo utandawazi au pengine hivi ndivyo wanavyofanya Wajerumani, Wamarekani na Waingereza! Maana hawa ndiyo waliotuletea eleimu na huko kwao ndiko tunakoiga mambo mengi likiwemo la elimu!

Kwa kasi hii ya kugawa shahada kila chuo, tusishangae shule za Kata zikaanza kutoa shahada kwa wanafunzi wake?  Napata taabu sasa kutambua umuhimu wa Vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Saint Augustine, Staint John, Tumaini, Chuo Kikuu Huria, Muhimbili, IMMTU, Chuo Kikuu cha Dodoma na vingine tulivyo navyo. Tunavitofautishaje na hivi vingine?

Ni ukweli usiopingika kwamba vyuo vya kada ya kati katika sehemu mbalimbali duniani hupewa hadhi ya kutoa shahada kwa wahitimu wake (hata kama chuo husika hakina hadhi ya Chuo Kikuu). Hapa kwetu kasi ni kubwa ajabu. Na kasi hii inaacha shaka kama maandalizi ya kina hufanyika. Aidha kasi hii inaonesha dhahiri kwamba wanaoshindwa kuendelea na masomo baada ya kumaliza darasa la saba (ambao ndyo wengi) wanakuwa wameondolewa rasmi katika mfumo rasmi wa elimu hapa nchini. Tujiulize wanakwenda wapi?

Kwamba Watanzania tunaongezeka kwa kasi ni kweli. Ongezeko hili lingeenda sanjari na ongezeko la shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari (za kata?) vyuo vya kada ya kati pamoja na Vyuo Vikuu. Nilipomuuliza mwalimu wangu, kulikoni mhasibu anajivunia digrii badala ya CPA? Alinijibu kuwa tutawachanganya wote na kuanza kupembua kama pumba na mchele na kuona ni yupi anafaa wapi… anayestahili cheti tumpe, anayestahili stashahada tumpe, anaystahili shahada tumpe, hali kadhalika wa astashahada, wa shahada ya pili na wa uzamivu (PhD) na CPA tutawapa tu. Sikuwa na swali tena!

Veta ilianza vizuri! Kidogo kidogo imeanza kubadili mwelekeo. Sasa hivi huwezi tena kufikiria kujiunga na Veta kama huna cheti cha kidato cha nne. Tunairuhusu Veta kufanya hivi tukijua wazi kuna mtihani wa mchujo wa darasa la nne, kuna mtihani wa mchujo wa darasa la saba  na kuna mtihani wa mchujo wa kidato cha pili! Hawa watakwenda wapi? Wanasaidiwaje? Au ndiyo wameshatupwa nje ya mfumo rasmi wa elimu? NGOs na sekta binafsi zinaweza kujitahidi, lakini mkono wa serikali kwa hawa walipa kodi watarajiwa uko wapi? Wazazi tunashangilia kila chuo kutoa shahada na matokeo yake tunaongeza pia juhudi za kununua mitihani inayouzwa kama njugu ili mtoto aende chuo “chochote” apate shahada! Hapo ndiko tulikofikia.

Wadau tusaidiane kuuweka bayana mfumo mzima wa elimu hapa nchini. Ni aibu hata pale anapoulizwa mdau au mamlaka zinazohusika kuelezea japo kwa kifupi mfumo wa elimu hapa nchini,  anapata taabu kweli kweli! Sana sana anaanza kuchomeka maneno ya kimombo alimradi tu kumchanganya muuliza swali pamoja na wasikilizaji. Kumbe ni jambo lililotakiwa kuwa wazi kwa kila mtu na linaloelezeka kwa urahisi tu. Nachelea kuzungumzia vyuo binafsi vinavyotoa vyeti na diploma. Kuna vyuo ukisoma hata miezi sita tu unapewa diploma, mwaka mmoja unapewa diploma, miaka miwili unapewa diploma! Mfumo uko je? Je diploma ya chuo kimoja na ya chuo kingine zinapimwaje? Utitiri wa vyuo vya teknolojia ya mawasiliano na vyuo vya ufundi usitufikishe mahali tukaanza kutoa diploma za uuguzi za miezi mitatu. Wallahi wa abillahi tutamalizana!

Ni wakati wa kutafakari juu ya mustakabali wa mfumo mzima wa elimu hapa nchini. Je, elimu ya msingi iishie darasa la saba au kidato cha nne? Tuige mifumo ya elimu ya majirani zetu? Tutafakari. Hatujachelewa sana!

0713 123 254