Wednesday, June 27, 2012
Tuesday, June 26, 2012
Bungeni Dodoma
Hii ni picha iliyopigwa na mwandishi mkongwe Manyerere Jacton akitaka kuuhadaa na kuupotosha umma kuhusu eneo ambalo waandishi wa habari hulitumia wakati wa mikutano ya Bunge Dodoma.
|
Huu ndiyo ukumbi rasmi kwa ajili ya waandishi wa habari za Bunge wawapo Dodoma. Wengi hawapendii kuutumia kutokama na kutokupende kupanda ngazi. |
Monday, June 25, 2012
Habari Mchanganyiko
Tuesday, June 12, 2012
Kada ya kati imesahaulika?
Na Prosper Minja
KATIKA makala yangu ya “Elimu kwa
vitendo shuleni iko wapi?” iliyochapishwa kwenye gazeti hili la Raia Mwema la
Mei 16 –Mei 22, 2012 toleo namba 239 watu wengi waliichangia mada hiyo.
Nawashukuru kwa kutoa mawazo mazuri ya kutaka kuondokana na ujenzi wa taifa la
walemavu wa viungo na akili. Makala ya leo bado inajikita tena katika eneo hili
la mfumo wa elimu Tanzania.
Katika miaka ya
hivi karibuni Tanzania inashuhudia mabadilko makubwa katika mfumo mzima wa
elimu unaosukumwa na utandawazi. Tofauti na ilivyozoeleka, vyuo vya elimu vya kada
ya kati vilivyokuwa vimeanzishwa kwa makusudi maalum sasa vinapoteza ule umaana
wake uliokuwa umekusudiwa. Sina hakika
sana na mfumo mzima wa elimu hapa nchini kwa sasa, ila wadau wenye uelewa
naomba tusaidiane katika hili.
Baada ya
Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, vilianzishwa vyuo mbalimbali kwa ajili ya
kada ya kati. Vilianzishwa vyuo vya elimu ya Ufundi magari/mshine, Uashi, Usimamizi
wa Fedha, Elimu ya Bishara, Ufundi Mchundo, Uhazili, Ustawi wa Jamii, Kilimo,
Mifugo, Uvuvi, Sanaa,Useremala, msururu ni ndefu. Chuo KIkuu kilianzishwa
kimoja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hiki kwa wakati na mazingira ya wakati wa
ule kilikidhi mahitaji ya watanzania na nje ya Tanzania.
Tayari mfumo wa
elimu ulikwishawekwa bayana. Mtoto ataanzia shule ya awali (chekechea),
atakwenda shule ya msingi kwa maana ya darasa la kwanza hadi darasa la saba
(enzi za mkoloni ilikuwa ni la nne) na hapa kwa vyovyote vile si wote wangeweza
kuendelea na masomo ya sekondari kwa maana ya kidato cha kwanza (au darasa la
tano kwa enzi za mkoloni). Vyuo vya kada
ya kati viliandaliwa mahususi kuwapokea hawa
wasioweza kuendelea na masomo ya sekondari ambao katika hali yoyote ile
ni wengi kwa kulinganisha na wale waliokwenda kwenye shule za sekondari.
Halikadhalika si
wote waliomaliza kidato cha nne walioweza kuendelea na kidato cha tano. Sanjari
na wazo la awali vyuo vya kada ya kati
vilikuwa vimeandaliwa kulipokea kundi hili pia ambalo kwa vigezo vyovyote ni
kundi kubwa na lenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kutenda. Na ni katika mantiki
hiyo pia tunakubaliana tena kwamba si wote waliomaliza kidato cha sita waliweza
kuendelea na masomo ya chuo kikuu. Ifahamike hapa kuwa swala kubwa ni uwezo wa
kuyamudu masomo na si vinginevyo. Kundi hili nalo lilipata nafasi katika vyuo
vya kada ya kati. Hii iliwezekana kwa kuwa tangu zama hizo hadi sasa mfumo wa elimu kuanzia chini hadi juu una
umbo la pyramid: kwa maana kwamba unavyokwenda
juu idadi ya wanafunzi inazidi kupungua. Huu ndiyo ukweli na hakuna jinsi ya
kuupinda au kuuchakachua.
Vyuo vya kada ya
kati vilitoa vyeti mbali mbali vilivyomtambullisha mhitimu pamoja na kazi
anayoweza kuimudu.Leo maandalizi ya kada hii ya kati yanapoteza mwelekeo. Sina
hakika kama msisitizo wa kujenga vyuo vya namna hii upo tena. Huenda msukumo
huu umeelekzwa kwa sekta binafsi. Lakini tukumbuke kwamba sekta binafsi lengo
lake ni kufanya biashara na kupata faida na si vinginevyo. Vyuo hivi vilikuwa
vinabeba mzigo mkubwa kuliko vyuo vikuu vyote hapa nchini tukivichanganya
pamoja.
Matokeo yake
kila chuo cha kada ya kati sasa hivi kinataka kusomesha na kutoa shahada
(degree) kwa wanafunzi wake. Kuanzia Hombolo, Mipango, Ustawi wa Jamii, Ufundi,
Usimamizi wa Fedha, Elimu ya Biashara, Kilimo, msrururu ni mrefu - vimeruhusiwa
kutoa shahada za Chuo Kikuu! Kesho akija mtu ofisini kuomba kazi atakupa cheti
cha shahada ya kwanza ya useremala kutoka Chuo (Kikuu?) cha Mbuyuni! Wote hawa
sasa wana shahada za vyuo vikuu!
Tulichekelea
watoto wa chekechea walipoanza kuvaa majoho “wanapohitimu”! Leo hii kila
anayehitimu chochote anataka na tunamshangilia akilivaa joho! Nasema nisaidieni
pengine huu ndiyo utandawazi au pengine hivi ndivyo wanavyofanya Wajerumani,
Wamarekani na Waingereza! Maana hawa ndiyo waliotuletea eleimu na huko kwao
ndiko tunakoiga mambo mengi likiwemo la elimu!
Kwa kasi hii ya kugawa
shahada kila chuo, tusishangae shule za Kata zikaanza kutoa shahada kwa
wanafunzi wake? Napata taabu sasa kutambua
umuhimu wa Vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Saint Augustine, Staint John, Tumaini,
Chuo Kikuu Huria, Muhimbili, IMMTU, Chuo Kikuu cha Dodoma na vingine tulivyo
navyo. Tunavitofautishaje na hivi vingine?
Ni ukweli
usiopingika kwamba vyuo vya kada ya kati katika sehemu mbalimbali duniani
hupewa hadhi ya kutoa shahada kwa wahitimu wake (hata kama chuo husika hakina
hadhi ya Chuo Kikuu). Hapa kwetu kasi ni kubwa ajabu. Na kasi hii inaacha shaka
kama maandalizi ya kina hufanyika. Aidha kasi hii inaonesha dhahiri kwamba
wanaoshindwa kuendelea na masomo baada ya kumaliza darasa la saba (ambao ndyo
wengi) wanakuwa wameondolewa rasmi katika mfumo rasmi wa elimu hapa nchini.
Tujiulize wanakwenda wapi?
Kwamba
Watanzania tunaongezeka kwa kasi ni kweli. Ongezeko hili lingeenda sanjari na
ongezeko la shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari (za kata?) vyuo
vya kada ya kati pamoja na Vyuo Vikuu. Nilipomuuliza mwalimu wangu, kulikoni
mhasibu anajivunia digrii badala ya CPA? Alinijibu kuwa tutawachanganya wote na
kuanza kupembua kama pumba na mchele na kuona ni yupi anafaa wapi… anayestahili
cheti tumpe, anayestahili stashahada tumpe, anaystahili shahada tumpe, hali
kadhalika wa astashahada, wa shahada ya pili na wa uzamivu (PhD) na CPA tutawapa
tu. Sikuwa na swali tena!
Veta ilianza
vizuri! Kidogo kidogo imeanza kubadili mwelekeo. Sasa hivi huwezi tena
kufikiria kujiunga na Veta kama huna cheti cha kidato cha nne. Tunairuhusu Veta
kufanya hivi tukijua wazi kuna mtihani wa mchujo wa darasa la nne, kuna mtihani
wa mchujo wa darasa la saba na kuna
mtihani wa mchujo wa kidato cha pili! Hawa watakwenda wapi? Wanasaidiwaje? Au
ndiyo wameshatupwa nje ya mfumo rasmi wa elimu? NGOs na sekta binafsi zinaweza
kujitahidi, lakini mkono wa serikali kwa hawa walipa kodi watarajiwa uko wapi?
Wazazi tunashangilia kila chuo kutoa shahada na matokeo yake tunaongeza pia
juhudi za kununua mitihani inayouzwa kama njugu ili mtoto aende chuo “chochote”
apate shahada! Hapo ndiko tulikofikia.
Wadau tusaidiane
kuuweka bayana mfumo mzima wa elimu hapa nchini. Ni aibu hata pale anapoulizwa
mdau au mamlaka zinazohusika kuelezea japo kwa kifupi mfumo wa elimu hapa
nchini, anapata taabu kweli kweli! Sana
sana anaanza kuchomeka maneno ya kimombo alimradi tu kumchanganya muuliza swali
pamoja na wasikilizaji. Kumbe ni jambo lililotakiwa kuwa wazi kwa kila mtu na
linaloelezeka kwa urahisi tu. Nachelea kuzungumzia vyuo binafsi vinavyotoa
vyeti na diploma. Kuna vyuo ukisoma hata miezi sita tu unapewa diploma, mwaka
mmoja unapewa diploma, miaka miwili unapewa diploma! Mfumo uko je? Je diploma
ya chuo kimoja na ya chuo kingine zinapimwaje? Utitiri wa vyuo vya teknolojia
ya mawasiliano na vyuo vya ufundi usitufikishe mahali tukaanza kutoa diploma za
uuguzi za miezi mitatu. Wallahi wa abillahi tutamalizana!
Ni wakati wa
kutafakari juu ya mustakabali wa mfumo mzima wa elimu hapa nchini. Je, elimu ya
msingi iishie darasa la saba au kidato cha nne? Tuige mifumo ya elimu ya majirani
zetu? Tutafakari. Hatujachelewa sana!
0713 123 254
Subscribe to:
Posts (Atom)