.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

.

.
.

Wednesday, March 21, 2012

Elimu kwa vitendo shuleni iko wapi?

Na Prosper Minja

KATIKA moja ya hotuba za hayati  Baba wa Taifa Mwlimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuna baadhi ya mambo hapa nchini ukitaka kuyahoji lazima uwe na moyo mgumu kama wa mwendawazimu hivi.   Kwa sasa moja ya mambo hayo ni elimu: elimu ya awali; elimu ya msingi; elimu ya sekondari; elimu ya vyuo. Zamani ili shule ihesabike  na hata kusajiliwa kama shule kuna mambo mengi yalihitajika likiwemo la uwanja wa michezo na shamba la shule. Siku hizi ni dhambi ya mauti kuzungumzia shamba la shule tena mzazi akikuskia achilia mbali mwalimu! Mwanafunzi ndiyo kabisa atatamani umwagiwe tindikali!
Siku hizi mtoto anafanyiwa kila kitu awapo shuleni. Kuna watu wa kufanya usafi ndani na nje ya vyumba vya madarasa, , kupika, basi la kumbeba na kurudisha nyumbani, akifika nyumbani kuna msaidizi/mfanyakazi wa nyumbani wa kumfulia hadi nguo za ndani, kumpikia, kumtandikia kitanda na kunyooshea nguo. Shuleni shamba darasa tena hakuna. Zamani katika orodha ya vifaa vya kwenda navyo shuleni jembe kilikuwa kifaa kimojawapo. Siku hizi dhubutu! Kiwanja cha michezo si sharti muhimu tena. Hali hii iko tangu shule ya awali hadi chuo kikuu! Ni dhahiri maandiko haya hayatabadilisha chochote kwa wakati huu lakini yataonekana ya maana Wachina watakapoanza kuchangamkia hata kazi za majumbani hapa Tanzania kwani wao wamefundishwa maana ya kazi kwa vitendo.
Serikali, wazazi, wadau wako wapi kudai na kuhimiza kazi za mikono katika shule zetu? Shule yoyote kabla ya kusajiliwa ioneshe japo shamba darasa mahali wanafunzi watajifunza kwa vitendo kupanda na kuvuna mchicha. Wanafunzi wafundishwe kufanya usafi kwa vitendo kwa mfano kufagia darasa, kuokota takataka, kukata kucha, kuosha sahani yake anapomaliza kula,  kutoa buibui na nyinginezo. Wakiwa majumbani wajifulie ngou zao wenyewe, wafanye usafi, wajifunze kupika, wanyooshe nguo zao wenyewe, watengeneze bustani na kuzimwagilia inapobidi, wahimizwe maswala ya kiroho, kwa kifupi wafundishwe kuwajibika.
Jeshi la Kujenga Taifa ndilo lilikuwa limesalia ili kuziba ombwe hili. JKT halipo tena. Na hata ikitokea likawepo halitokuwa tena kama la opereshini miaka 30 (waliopita jeshini wanaelewa operesheni).   Ole wetu! Ole wa Taifa hili!. Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt. Ndalichako alinukuliwa akilalamika kwamba wanafunzi waliandika mashairi ya Bongo flavor kwenye mitihani! Kumbe waandike nini? Nyimbo za makuzi shuleni siku hizi hakuna tena. Nyimbo za kizalendo na ukakamavu ni historia mashuleni! Kibaya zaidi hata Wimbo wa Taifa  umebaki kuchezwa mkanda tu uliorekodiwa halafu  wanafunzi kusikiliza! Mustakabali wa Taifa uko wapi! Tusipojenga msingi imara tusishangae nyumba kuporomoka kwani Walatini wanasema volenti non fit injuria! (lakijitakia halina madhara). Tumeyata wenyewe!
Tuna wakaguzi waliosoma. Hivi hawa wanakagua nini? Mwandiko mzuri? Mwalimu kumaliza silabasi? Wadau nisaidieni. Mada ni pana. Mtoto huyu akimaliza shule (darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita, shahada ya kwanza) anakuwa ni mzigo usiobebeka pande zote. Si kwa wazazi, si kwa serikali! Hawezi kufanya kitu chochote! Hajafundishwa kufanya hivyo! Hajalelelwa katika mazingira hayo! Hana pa kuanzia. Dhana ya kilimo kwanza kwake ni msamiati usio na mashiko. Likitokea la kutokea kwamba mzazi amefariki dunia huu unakuwa ni mwanzo wa mwisho wa mtoto huyu! Ataanza kujioanisha na mazingira  yatakayomfaa (to search for identity). Atayapata mazingira hayo  au kwa watumia dawa za kulevya kwa wavulana au kwa kupiga umalaya kwa wasichana. Hapa tusiulizane madhara yake nini.
Laiti mtoto huyu angelikuwa anajua kujitegemea japo kidogo tu angeyamudu maisha. Angekuwa mnyenyekevu. Kwa bahati mbaya kila mtoto anaota kwenda Ulaya tena kwa gharama yoyote ile. Mzazi atafanya kila linalowezekana na lisilowezekana, mtoto atahonga hata visivyohongeka ili mradi aende Ulaya! Kufanya nini? Sina jibu.
Sera ya elimu iangaliwe upya. Shule zote (binafsi na serikali) ziwekewe vigezo. Tusiogope kujifunza kutoka mahali pengine. Kwa mfano shule za seminari zinaongoza kwa kufanya vizuri. Lakini hapa ni mahali wanafunzi wanafanya kazi zote peke yao. Wana mashamba yao wanayolima na kuvuna wenyewe, wanafanya usafi wa mazingira na vyumba vya madarasa yao, kwa kifupi wanajitegemea wakiongozwa na nidhamu ya hali ya juu. Haijawahi kutokea mtoto aliyemaliza masomo katika shule hizi akawa tegemezi kiasi cha kutobebeka. (kwa ujasiri naruhusu changamoto/challenge kwa hili kutoka wa mtu yeyote). Huu ni ushahidi kwamba inawezekana.
Tujenge msingi imara ili kuwa na taifa imara.
0713 123 254
www.prince-minja.blogspot.com
 (Tanzania Daima, Na. 2665, Machi 21, 2012, uk 20)